WADAU WA MAENDELEO KUCHAGIA BILIONI 98.1 KUPITIA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA
Na.WAF-Dar es Salaama
Wadau wa Mfuko wa Afya wa pamoja nchini (Health Basket Fund) wamepanga kuchangia kiasi cha shilingi Bilioni 98.1 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2022/2023.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha kujadili uboreshaji wa mfuko huo kupitia ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau Jijini Dar Es Salaam.
“Kwa niaba ya Serikali tunawashukuru wadau wetu wanaochangia kwa pamoja kwenye Mfuko wa Afya na tunatarajia kwa Mwaka wa fedha ujao wa 2022/23 wadau wetu kwa pamoja kuchangia Shilingi Bilioni 98.1 na fedha hizo zitaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema katika mwaka wa fedha uliopita wadau kupitia Mfuko walichangia kiasi cha shilingi bilioni 74.3 ambapo asilimia 90 ya fedha zimekwenda kwenye Halmashauri na zimeingizwa moja kwa moja kwenye Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya nchini.
Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia Mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.
“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweke kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja,
mapendekezo yetu wadau wengine wachangia kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu